
RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesisitiza kauli yake ya
kuwataka viongozi na watendaji katika sekta ya umma kuacha kufanya kazi
kwa mazoea huku akieleza azma ya serikali ya kuwaongeza mshahara
wafanyakazi wa kima cha chini ifikapo Aprili mwaka huu kuwa iko pale
pale.
Aliyasema hayo kwenye Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, Mnazi
Mmoja mjini Unguja wakati akifunga semina ya siku moja kwa viongozi na
watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuhusu umuhimu wa
takwimu na matumizi yake.
Alisisitiza haja kwa kila kiongozi kuhakikisha anasimamia vyema kazi
zake pamoja na kuwasimamia anaowaongoza katika sehemu yake ya kazi
pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kuachana na kufanya kazi kwa mazoea.
Alisema ni jukumu la kila kiongozi kubadilika katika utendaji wake wa
kazi na kuwataka wajitahidi kufanya hivyo licha ya kuwa itachukua muda,
lakini aliwasisitiza kuwa si busara kuendelea kufanya kazi kwa mazoea.
Dk Shein alisema moja kati ya tamko la Ilani ya Chama cha ASP katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1963 ilikuwa ni kuwapa nafasi Waafrika wa
Zanzibar kuongoza nchi yao na baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964
chini ya uongozi wa Mzee Abeid Amani Karume hilo lilifanikiwa kwa
kuanzia Wizara ya Afya na kuendelea kwa wizara nyingine ambapo wananchi
wa Zanzibar walipata fursa ya kufanya kazi.
0 comments:
Post a Comment