
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Freeman Mbowe amekutana kwa dharura na mameya, manaibu meya na viongozi
waandamizi kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
wa Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili suala la Shirika la Usafiri Dar
es Salaam (UDA).
Hivi karibuni, Rais John Magufuli wakati akizindua Mradi wa Mabasi
yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam (DART) alitoa siku tano kwa uongozi
wa Jiji kuhakikisha Sh bilioni 5.8 zilizolipwa na Kampuni ya Simon
Group zinapangiwa matumizi baada ya kuuzwa hisa asilimia 51 kati ya 100
kwa kampuni hiyo.
Jiji la Dar es Salaam kwa sasa linaongozwa na Ukawa chini ya Meya kutoka
Chadema, Isaya Mwita. Katika kikao cha baraza Halmashauri ya Jiji hilo
chini ya Meya Mwita kilichofanyika wiki iliyopita, kilishindwa kufikia
mwafaka wa kuzipangia matumizi fedha hizo kutokana na madai ya wajumbe
wa baraza hilo kuwa kitendo hicho ni kubariki ufisadi wa kuuza hisa kwa
Simon Group.
Kikao hicho cha Baraza kilifanyika ili kuitikia agizo hilo la Rais Magufuli alilolitoa wakati wa uzinduzi wa mradi wa Dart.
Hata hivyo, pamoja na siku tano alizotoa kuisha bado halijapatiwa
ufumbuzi. Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni,
alipozungumzia suala hilo nje ya ukumbi wa Bunge, alikiri kuwaita
viongozi hao wa jiji la Dar es Salaam ili kuzungumzia suala hilo la UDA.
“Nimewaita ili tuzungumze sintofahamu ya suala hili ili tupate msimamo
wa pamoja.Tunahitaji kupata suluhisho la suala hili ili wakazi wa Dar es
Salaam wanufaike na Uda,” alisisitiza.
Katika jiji la Dar es Salaam lenye halmashauri sita, Ukawa ilishinda
halmashauri tatu ikiwemo halmashauri ya jiji hilo inayoongozwa na Mwita,
Ubungo ikiongozwa na Boniface Jacob na Ilala chini ya Charles Kuyeko.
Baadhi ya viongozi hao wa Ukawa wa Dar es Salaam walionekana
wakirandaranda katika viwanja vya Bunge jana na baadhi yao walikiri
kuitwa na mwenyekiti huyo wa Chadema huku wakidai kuwa hawafahamu
wameitiwa nini.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), George Simbachawene akizungumzia kushindwa kugawanywa kwa
fedha hizo alitaka watendaji wa jiji hilo wapewe muda ili waweze kuja na
suluhisho la suala hilo.
Alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia maagizo ya Rais Magufuli kuhusu
matumizi ya fedha hizo, lakini endapo atapewa maelekezo kuhusu fedha
atayatekeleza.
0 comments:
Post a Comment