HAKUNA aliyeaibika wakati akijaribu kufanya jambo kwa faida yake. Siku
zote kufanya jaribio ni mwanzo wa kuelekea kwenye ufanisi mzuri wa jambo
husika.
Rafiki zangu, ni vema nawe ukajiwekea utaratibu wa kujaribu kufanya
mambo ambayo unadhani huyawezi, lakini yakileta matokeo chanya yatakuwa
na faida kubwa kwako.
Kujaribu kupo katika mambo mengine mengi ya kawaida – ya kibinadamu.
Katika mambo mbalimbali ya kila siku. Ukianza na kupata matokeo mazuri,
unakuwa mshindi na bila shaka unakuwa umefanikiwa.
Hali ni tofauti katika suala la mapenzi, huku hakuna kujaribu – ni
kuamua tu! Hata hivyo, wakati unaamua mambo yako yanayohusu mapenzi ni
lazima kichwani mwako utambue kuwa unafanya kitu kwa ajili yako na mtu
mwingine (mpenzi wako).
Hapo ndipo kazi inapokuja. Kwa maneno mengine, wakati ukijifikiria wewe
katika ulimwengu wa mapenzi, unatakiwa pia kumfikiria mpenzi wako.
Kwa bahati mbaya, katika eneo hili, wanaume wengi huwa hawafikirii sana
namna ya kuwafurahisha wenzi wao. Wanahisi ni suala linalowahusu
wanawake pekee. Ni kosa.
Kama mwanaume lazima upate wakati wa kujua unatakiwa kufanya nini kwa ajili ya kulifanya penzi lako lizidi kuchanua.
Hapa katika Love Moment, nimekuandalia mambo ambayo wanawake wengi wanavutiwa zaidi kutoka kwa wanaume.
Je, wewe ukoje? Una sifa hizo? Hebu twende pamoja katika mada hii ambayo bila shaka itakutoa matongotongo.
USAFI BINAFSI
Asilimia kubwa ya wanawake wanapenda sana usafi. Ni aghalabu sana
kukutana na mwanamke asiyejipenda. Ndiyo maana wanaitwa mapambo ya
nyumba au ua la nyumba! Ni kwa sababu ya hulka yao ya kupenda sana
usafi.
Mwanamke anavutiwa sana na mwanaume mtanashati. Usafi wako unamfanya
ajiamini kuwa na wewe. Hata nyumbani kwako, lazima uishi katika nyumba
safi. Hata anapokuja kukutembelea, anakuta mazingira masafi kuanzia
sebuleni hadi chumbani.
Anapokukuta katika hali ya usafi, inakuwa rahisi zaidi yeye kuanzia hapo alipokukuta na kuendelea mbele.
KUJIAMINI
Mwanamke anajisikia salama zaidi akiwa na mwanaume ambaye anajiamini –
mwenye uwezo wa kutetea hoja zake na kujieleza sawia. Siyo anayebabaika.
Suala la msimamo binafsi, kwa mwanamke ni kubwa kuliko hata kumnunulia
manukato mapya. Mathalani unakuwa naye katika mtoko, angependa kukuona
ukiwa katika hali halisi ya maisha yako, usiyeyumbishwa na mwenye kutoa
maamuzi yasiyoyumba.
Wakati mwingine, mwanamke anaweza kukupima hata katika jambo ambalo
amekosea yeye, ataangalia unavyotoa maamuzi yako, lakini pia atafuatilia
kuona kama utakuwa mwepesi wa kuyabadilisha.
Anataka kuona msimamo wako muda wote. Mwenye kujiamini na mawazo yasiyo na matege wala makengeza!
KUJITETEA
Kipengele hiki hakina tofauti kubwa sana na kilichopita, lakini hapa ni
kwenye upande wa kujitetea zaidi. Wakati unapodai haki yako mbele ya
mwanamke wako, suala la kujitetea linapewa nafasi kubwa sana.
Wanawake hawapendi kuwa na wanaume ambao wapo tayari kuonewa. Wanataka
wenye uwezo wa kusimama kidete kuona haki zao hazichukuliwi kirahisi.
Hili si suala la kutetea tu haki yako pekee kama mwanaume, bali
inapobidi kusimamia haki ya mwanamke wako. Nisieleweke vibaya katika
hili, lakini mwanaume imara ni yule ambaye ana nguvu – anafanya mazoezi
na ambaye yupo tayari kwa lolote!
Inapowezekana, uwe na uwezo wa ‘kuzichapa’ ikiwa mtakutana na vibaka au
watu wabaya wenye lengo wa kukudhuru/kuwadhuru au kumdhuru mpenzi wako.
Mwanaume aliye ‘fiti’ ni chaguo la wanawake wengi. Si mnyonge. Mpole kupitiliza na aliye tayari kuonewa! Huyu hana nafasi.
KUJALI
Wanawake wanapenda sana wanaume wanaojali. Wanawaona wao ni kila kitu na
wanaotoa kipaumbele kwao. Kama huna tabia hiyo, ujue upo katika nafasi
kubwa ya kumkwaza mpenzi wako. Mjali mpenzi wako kwa kila hali.
Kumjulia hali kila wakati na kutaka kujua maendeleo yake, kutakupa nafasi kubwa sana ya kuendelea kudumu katika uhusiano hai.
UKARIBU
Kati ya vitu vinavyowapa mshawasha mkubwa wanawake ni pamoja na
kusogezwa karibu. Hapa ni kuwa naye katika mambo mengi unayoyafanya kila
siku.
Ni vizuri kuwasiliana naye mchana, ukitaka kujua aina ya chakula
alichokula siku hiyo au ikiwezekana mchagulie. Ni mambo madogo sana
lakini yanayoongeza nakshi katika mapenzi.
Yapo mengi sana ambayo kwa kuyafanya utakuwa umemsogeza mpenzi wako
karibu yako. Hebu tumia ubunifu wako ili uweze kuteka hisia za mwenzi
wako kisawasawa.
0 comments:
Post a Comment