NINA hasira kama nini hapa mnaponiona, yaani nimevurugwa kabisa.
Mwenyewe nilijua timu yangu ndiyo tunachukua ubingwa msimu huu, mara eti
katimu hakana hata historia na huu mchezo kamekuja kutuvurugia. Tangu
siku ile sijatoka ndani, maana jirani yangu alikuwa ameweka madebe
barazani anapiga ananisubiri! Kama siyo shoga yangu Ma Muhaji kuja
nidokeza kisa cha mke wa rafiki wa mwanaye wa kiume, basi nilitaka leo
niahirishe hili somo, nikae zangu ndani niendelee kusikilizia maumivu,
yanaumajeee!!
Basi, Mama Muhaji kaniambia, eti mke wa rafiki wa mwanaye kaondoka
nyumbani kwa ngoma, yaani kajaza watu akimtukana mumewe, matusi
makubwamakubwa na watu wanashangilia. Kijana wa watu, nasikia kakaa
kimya ndani, kavumilia mvua ya matusi na dharau, mwisho wa siku huyo
dada kachukua begi lake, akaondoka kwa mbwembwe, eti wataonana kuzimu!
Sasa alichonishangaza shosti, eti huyo bi dada kakaa huko alikokaa wiki
tatu tu, karudi anataka waendelee na maisha na kijana wa watu.
Kilichonifurahisha, mvulana kamwambia mkewe, yupo tayari kuendelea
kuishi naye ili mradi tu, ajaze watu kama alivyofanya siku ile
anaondoka, halafu awaambie kwa nyodo zilezile kwamba anataka kurudi!
Fyuutu, unadhani aliweza, akaishia kulialia na hadi jana anaondoka hapa
kwangu Ma Muhaji, hata hatujui nini kinaendelea, maana mjumbe kakataa
kwenda kusuluhisha, majirani wote hawataki na marafiki ndiyo kabisaa,
wenyewe kwanza wanaona aibu wakikumbuka shoga yao alivyokuwa akitamba
kwa pozi siku ile! Sasa kwa sababu hiyo ndo nimeona acha niwape kidogo
uzoefu, maana nyie wengine mnadhani kubadilisha wanaume, au kuwa wajeuri
ndiyo mnaonekana wajanja.
Kwanza shurti mjue, siku zote, pamoja na uzuri walionao, shepu zao na
hata majukumu yao, heshima ya mwanamke inatokana na mwanaume.
Asikudanganye mtu, achilia mbali kuolewa, ile tu kuishi na mwanaume
ndani, ni heshima tosha kwa mwanamke.
Ile inakuonyesha ni kwa kiasi gani wewe una baraka za Mwenyezi Mungu,
kwa sababu kuna wanawake na uzuri wao, hakuna mwanaume anafikiria kuishi
nao. Na wasikudanganye ukisikia wanasema hawana shida na mwanaume, ni
waongo. Mwanamke na hata awe na hela vipi, anaweza kutoka kwenye jumba
lake la kifahari, akamfuata mwanaume anayeishi mbavu za mbwa.
Ukimpata mwanaume, shikamana naye. Usije kufanya jambo kwa sababu ya
kutaka sifa kutoka kwa mashoga. Kwanza katika hao mashoga wanaoshangilia
unapomkosea adabu mwanaume wako, wangapi wanaishi na wanaume? Mwanamke
anayeishi na mume, hawezi kukuunga mkono kwenye ujinga huo, labda na
yeye awe hamnazo! Kitu kingine ambacho sisi wanawake tunakuwa hatujui ni
kwamba wenzetu wanaume, hata waache wanawake mara ngapi, hata
hawaonekani kuwa na dosari, lakini sisi sasa, eti umeachika mara tatu
tu, nakuambia hata kosa si lako utaonekana wewe ndiyo tatizo!
Ninachotaka mjue, kile kitendo tu cha mwanaume kukubali kukuweka ndani,
ni heshima kubwa sana.
Kuna maelfu ya mashoga huko mitaani wameshindwa kuwapata, tena wadada
wazuri, wanajiremba, wanavaa, lakini ndiyo wanaishia maisha ya klabu,
kila mwanaume anaguna ukimuambia amuweke ndani! Cha msingi, ukimpata,
kaa naye chini mrekebishane makosa, lakini jivunie kuwa naye! Kwa leo ni
hayo tu mashosti, tukutane wiki ijayo ni mimi Anti Nasra, Shangingi
Mstaafu!
0 comments:
Post a Comment