WAKATI Wizara ya Katiba na Sheria ikiingia rasmi katika ofisi zake mpya
mjini Dodoma jana baada ya kuhamia mwishoni mwa wiki, Wizara ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi nayo imetangaza kuhamia mjini humo wiki mbili zijazo,
huku ikiwatoa hofu watumishi wanaohamia huko kwa kuwataka kutekeleza
majukumu yao ipasavyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mathew Mtigumwe jana
aliwaondoa hofu watumishi wa wizara yake kuwa suala la kuhamia Dodoma
kuwa litafuata misingi na stahili za watumishi kwa mujibu wa kanuni za
utumishi wa umma.
Alitoa kauli hiyo wakati wa kikao maalumu kilicholenga kujadili kwa
pamoja namna ya utendaji kazi katika wizara hiyo sambamba na kutoa
utaratibu utakavyokuwa kuelekea kuhamia makao makuu ya nchi, Dodoma.
Alisema awamu ya kwanza ya uhamisho utahusisha watumishi 88 kutoka Idara
Kuu ya Mazao, watumishi 41 watahamia Dodoma kuanzia Februari 14 na 15,
mwaka huu huku wengine 47 watahamia muda wowote kati ya mwezi huu na
Juni mwaka huu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amezindua rasmi ofisi
za wizara Dodoma na kuwataka watumishi waliohamia kutekeleza majukumu
yao ipasavyo.
Makao Makuu ya wizara hiyo yaliyozinduliwa yapo katika Chuo Kikuu cha
Dodoma na tayari watumishi wa wizara hiyo 31 wamehamia rasmi wakiongozwa
na Dk Mwakyembe, Katibu Mkuu Profesa Sifuni Mchome, Naibu Katibu Mkuu
Amon Mpanju.
Awamu ya pili ya tatu zinatarajiwa kufuata utaratibu uliowekwa na
kufikia mapema mwakani, watumisho wote wa wizara hiyo watakuwa wamehamia
Dodoma.
Baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoa mwelekeo wa kuhamia makao
makuu ya nchi kwa makatibu wakuu, manaibu wao pamoja na mawaziri na
manaibu wao ifikapo Februari 28, mwaka huu, tayari wizara kadhaa
zimehamia ikiwemo ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora iliyohamia wiki iliyopita.
0 comments:
Post a Comment