Anne Kilango Aisimulia Siku Aliyotimuliwa Ukuu wa Mkoa..!!!!

Anne Kilango Malecela, ambaye wiki iliyopita aliteuliwa na Rais kuwa mbunge, amezungumzia yaliyomsibu tangu Oktoba 25 mwaka juzi alipopoteza ubunge, kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa kisha kutimuliwa hadi aliporudishwa bungeni, akisema yote yalikuwa mpango wa Mungu.
Kilango, aliyejinasibisha kama mpambanaji wa ufisadi wakati wa Bunge la Tisa, alipoteza ubunge wa Jimbo la Same Mashariki katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015 baada ya kuliongoza kwa miaka 10.
Miezi mitano baadaye, alifarijika baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli Machi 13 mwaka jana kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kuapishwa siku mbili baadaye.
Lakini, alitumikia wananchi wa mkoa huo kwa siku 27 tu baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wake Aprili 11 mwaka jana, baada ya Kilango kudaiwa kutoa takwimu za uongo kuhusu idadi ya watumishi hewa. Hata hivyo, baadaye Rais Magufuli akieleza sababu za kutengua uteuzi wake, aliahidi kumpangia kazi nyingine.
“Ndani ya nafsi yangu najua ule ulikuwa mpango wa Mungu,” alisema Kilango katika mahojiano maalumu.
“Wakati mwingine unaweza kuona jambo limekujia baya, kumbe ni Mungu anashusha nusura yake.”
Kilango alisema habari za kushindwa katika uchaguzi, kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa na kutenguliwa, alizipokea kwa kumshukuru Mungu akisema alijua kuna sababu ya hayo kutokea.
“Taarifa za kutenguliwa nilizipokea sawasawa na zile za kuteuliwa. Nilipoteuliwa nilimshukuru Mungu, vilevile, nilipotenguliwa nilimshukuru Mungu kwa sababu niliamini yote yaliyojiri yeye ndiye mhusika mkuu,” alisema.
“Mungu angetaka mpaka leo niwe mbunge wa Same Mashariki ningekuwa, angetaka pia niwe mkuu wa mkoa, Rais Magufuli asingenitengua.”

0 comments:

Post a Comment