Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesema dawa za
kulevya zinateketeza nguvukazi ya Taifa, jambo ambalo halipaswi kuachwa
liendelee kumea.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,
Sheikh Alhad amesema baraza la viongozi wa dini la kupambana na dawa za
kulevya nchini linaunga mkono juhudi zifanywazo na Serikali kupambana na
jambo hilo.
“Suala la matumizi ya dawa za kulevya limekuwa kikwazo cha maendeleo
nchini kutokana na nguvu kubwa ya Taifa ambayo ni vijana kujihusisha na
utumiaji wa dawa hizo,” amesema.
Amesema kuwa wanawataka viongozi wengine wa umma kuiga mfano wa Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wa kupambana na uovu wa uuzaji na
utumiaji wa dawa za kulevya ambao ni janga kwa Taifa.
“Tunawaomba wananchi wote kuunga mkono suala hili pamoja na kuonyesha
ushirikiano wa kutosha kwa wale walioamua kujitoa kwa ajili ya nchi
yetu.”
Katibu wa baraza la viongozi wa dini la kupambana na dawa za kulevya
nchini, Padri John Solomoni ameitaka Serikali kushughulikia suala hilo
kwa umakini ili lisiibue manung’uniko miongoni mwa wananchi ambao hawana
hatia.
Padri huyo amewataka viongozi wanaochunguza suala hilo kuwa makini ili wasiharibu haki ya mtuhumiwa.
“Ikumbukwe kwamba wanaotajwa ni watuhumiwa, huenda baada ya uchunguzi
wakabainika kuwa hawakuhusika. Baada ya kugundulika kuwa hawana hatia na
itakuwa vigumu kurudisha waliyokuwa nayo hapo mwanzoni,” amesema.
Kwa takriban wiki moja sasa, watu mbalimbali wamehojiwa na polisi
kuhusiana na ama utumiaji wa dawa hizo au uuzaji katika vita
inayoendeshwa na mkuu wa mkoa huo.
0 comments:
Post a Comment