“Usione vyaelea vimeundwa.” Huo ni msemo wa wahenga unaomaanisha kila mafanikio yana maandalizi yasiyo ya kubahatisha.
Msemo huo unaendana na kilichotokea katika matokeo ya mtihani wa kidato
cha nne yaliyotangazwa wiki hii, ambayo katika shule 10 zilizofanya
vizuri hakuna hata moja yenye maandalizi ya lele mama. Shule nyingi kati
ya hizo ada zake ni kuanzia Sh8 milioni hadi 10 kwa mwaka.
Uchunguzi umebaini kuwa shule hizo zote ni zenye majengo mazuri, walimu
wazuri na wenye motisha, maabara zilizokamilika, sehemu nzuri za kulala
na zinazotoza ada zaidi ya Sh2.5 milioni, mbali ya gharama nyingine za
chakula, malazi na vitabu.
Shule 10 zenye watahiniwa zaidi ya 40 zilizoshika nafasi za kwanza ni
Feza Boys (Dar es Salaam), St. Francis Girls (Mbeya), Kaizirege
(Kagera), Marian Girls (Pwani), Marian Boys (Pwani), St Aloysius Girls
(Pwani), Shamsiye Boys (Dar es Salaam), Anwarite Girls (Moshi),
Kifungilo Girls (Lushoto) na Thomas More Mashrina (Dar es Salaam).
Wanafunzi wa Sekondari Kaizirege Junior iliyoshika nafasi ya tatu, kila
mmoja analipa Sh2.5 milioni za ada. Malipo hayo kwa baadhi ya shule
hayahusishi gharama za malazi, chakula na vitabu.
Shule ya Wasichana ya St. Francis ili mwanafunzi ajiunge nayo,
anatakiwa kulipa Sh2.2 milioni za ada kwa mwaka, huku akitakiwa kulipa
katika mikupuo minne mbali na mahitaji mengine.
Mwanafunzi wa Feza Boys ada ni Sh2.9 milioni, lakini ikijumlishwa na
gharama za chakula, malazi na vifaa vya masomo, inafika zaidi ya Sh8
milioni.
Kuhusu Thomas More Machrine ada ni Sh3.6 milioni kwa kidato cha nne na
cha sita. Hivyo, mwanafunzi akisoma kwa miaka minne anatakiwa kulipa
Sh14.4 milioni.
Uchunguzi huo ulibaini mwanafunzi anayesoma shule za Marian Boys na
Girls kidato cha kwanza hadi cha nne, anatakiwa kulipa Sh2.8 milioni.
Kwa wanafunzi wanaojiunga na shule hiyo kwa ajili ya kidato cha tano na
sita, watalipa Sh2.7 milioni hiyo ina maana watatakiwa kulipa Sh5.4
milioni kwa miaka miwili.
Shule ya Anwarite ya Kilimanjaro ada yake ni Sh1.9 milioni, hivyo kwa miaka minne mwanafunzi analazimika kulipa Sh7.6 milioni.
Mmoja na viongozi wa shule hizo ambaye hakuwa tayari kutajwa, alisema
shule hizo zinatoa elimu bora na mazingira mazuri ya kuishi kwa
mwanafunzi, hivyo badala ya kuonekana kero zingepewa ruzuku.
0 comments:
Post a Comment