MGOGORO wa CUF umeendelea kupata sura mpya, baada ya upande wa
Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, kutoa kauli ikionesha hofu ya
usalama wao na ofisi za chama hicho Buguruni, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi hizo jana, Mkurugenzi
wa Ulinzi na Usalama wa CUF, Masoud Mhina alidai kuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Uongozi, Julius Mtatiro na wenzake, wamepanga kuvamia ofisi za
chama hicho.
Mhina alidai tayari walinzi wa chama wamejipanga kukabiliana na kikundi chochote chenye dhamira ya kuhujumu chama hicho.
“Tuna taarifa kuwa kuna vijana wanaandaliwa kuja kuvamia ofisi kuu za
chama Buguruni kwa ajili ya kufanya vurugu, nadhani wanatufahamu vizuri,
tukianza huwa hatukamatiki na tutahakikisha chama kinabaki salama,”
alidai.
Mhina alidai wanawafahamu viongozi waliopanga hujuma hizo na tayari
wamewasiliana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu vitisho na vitendo
vya udhalimu vinavyokusudiwa kufanywa na wasaliti wa chama hicho, dhidi
ya viongozi wa chama upande wa Bara.
Alidai kwa sasa hawawezi kuweka wazi majina ya viongozi hao kwa kuwa
wanajijua na vikao wanavyofanya kila kukicha ila ipo siku watawataja
ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria na kikatiba.
“Tutawashughulikia kisheria na kikatiba wanaotaka kuhujumu chama kokote
waliko tutawatafuta hadi maeneo ambayo wanafanyia mikutano na
kuwakamata, maana CUF hatuna mgogoro, ulishamalizwa na Msajili wa Vyama
vya Siasa,” alidai.
Mhina alitoa onyo kwa wanaojiita viongozi wa CUF wanaozungumzia
vichochoroni na kuwataka kama ni halali, waache na badala yake waende
ofisi za chama hicho ili wamweleze Profesa Lipumba walipewa uongozi na
nani.
“Tumewavumilia sana kiasi cha kutosha, sasa dawa yao ipo jikoni mmoja
mmoja baada ya mwingine tutawajibika nao, hivyo nachukua nafasi hii
kutoa onyo kwao kama ni viongozi, bora waje ofisini si kuzungumzia
vichochoroni,” alisema.
Awali akizungumzia kazi za Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Chama, Mhina
alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF ibara ya 88 (2) (a), Katibu atakuwa
Mtendaji Mkuu wa Kamati na Ibara ya 87 (1) imeeleza kuwa wajibu wa
Kamati hiyo ni kuhakikisha usalama wa chama unakuwapo nchini.
Alitumia nafasi hiyo kumsihi Katibu Mkuu aache vikao vya kuhujumu chama,
kwa kuwa havina tija kwake zaidi ya kujenga uhasama dhidi ya wanachama
na viongozi hao Bara na Zanzibar.
Akizungumzia tuhuma hizo, Mtatiro alihoji kuwa tangu lini Mwenyekiti wa
Chama akachaguliwa na Msajili na kuongeza kuwa Buguruni pamejaa wahuni
wanaomlinda Lipumba, hivyo hawawezi kufika eneo hilo.
“Hatuwezi kufanya upuuzi kama huo wa kwenda pale na hakuna anayetaka
kuvamia, kwa kuwa hakuna anayetaka kukaa kwenye ofisi ile kimabavu kama
Lipumba, tena kwa msaada wa wahuni na Polisi, sasa tunakwenda kuhujumu
nini na ili iweje?”Alihoji.
Alihoji wanaojiita wakurugenzi, wameteuliwa na nani wakati hawamtambui Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF.
Kwa mujibu wa Mtatiro, ili mtu awe Mkurugenzi lazima ateuliwe na
Mwenyekiti halali wa chama anayetambuliwa na vikao vya kitaifa hivyo
haelewi waliteuliwa na nani.
0 comments:
Post a Comment