SERIKALI imefanya tathmini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula
nchini na kubaini kwamba uzalishaji wa chakula nchini utakuwa na ziada
ya tani 3,013,515.
Akisoma kauli ya serikali kuhusu hali ya chakula na lishe nchini katika
mwaka 2016/17 bungeni Dodoma jana, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk
Charles Tizeba alisema tathimini iliyofanywa, imebaini kwamba jumla ya
tani 35,491 za chakula zinahitajika katika kukabiliana na hali ya
upungufu wa chakula na lishe kati ya Februari na Aprili mwaka huu kwa
ajili ya watu 1,186,028 walioainishwa kuwa na upungufu katika
halmashauri 55.
Kwa mujibu wa Dk Tizeba, ziada hiyo ilibainika baada ya Bunge la 10
kutoa kauli ya kufanya tathmini ya upatikanaji na mahitaji ya chakula
ambapo tathmini ya awali ya uzalishaji chakula kwa mwaka 2015/16 na
upatikanaji wa chakula mwaka 2016/17, ilikamilika.
Alieleza kuwa tathmini hiyo ilionesha kuwa kitaifa, uzalishaji wa
chakula utafikia tani 16,172,841 za chakula na mahitaji ya chakula kwa
mwaka huo ni tani 13,159,326 na hivyo kuwa na chakula cha ziada cha tani
3,013,515 yaani tani 1,101,341 ni mazao ya nafaka na tani 1,912, 174 ni
za mazao yasiyo ya nafaka.
Aliongeza kuwa nchi ilikuwa na utoshelevu wa chakula kwa asilimia 123,
lakini pamoja na hali nzuri cha chakula kitaifa, kulikuwa na halmashauri
43 ambazo zilikuwa na maeneo yenye upungufu wa chakula.
Aliongeza kuwa tathmini hiyo ilishirikisha Shirika la Kilimo na Chakula
Duniani (FAO) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na wataalamu kutoka
Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)
pamoja na Wizara ya Afya kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC).
Alieleza kuwa tathmini hiyo ilizingatia mihimili minne ya usalama wa
chakula ambayo ni upatikanaji wa chakula, ufikiwaji wa chakula, utumiaji
wa chakula na uthibiti wa chakula, ilitumia mfumo wa uainishaji
madaraja ya usalama wa chakula na lishe.
Aidha, alisema Serikali inafuatilia mwenendo wa bei za mazao ya chakula
hususani mahindi, mchele na maharage ili kujiridhisha uwepo wake sokoni.
Tathmini imebaini jumla ya tani 35,491 za chakula zinahitajika katika
kukabiliana na hali ya upungufu wa chakula na lishe kati ya Februari na
Aprili mwaka huu kwa ajili ya watu 1,186,028 walioainishwa kuwa na
upungufu katika halmashauri 55. Aidha, watu 118,603 wasio na uwezo wa
kupata chakula watahitaji tani 3,549 za chakula cha bei nafuu haraka.
0 comments:
Post a Comment