KUPELEKWA wanafunzi waliopata alama za chini katika mtihani wa darasa la
saba na hivyo kushindwa kumudu masomo ya sekondari, kumetajwa kuwa ni
moja ya sababu za kufanya vibaya kwa shule sita za Mkoa wa Dar es Salaam
katika matokeo ya Kidato cha Nne mwaka jana.
Mbali ya hilo, imebainika kuwa viashiria vya matokeo mabaya kwa shule
hizo vilianza kuonekana katika matokeo ya mtihani wa majaribio, jambo
ambalo liliwafanya wakurugenzi kuwaandikia barua wakuu wa shule hizo
kuongeza juhudi katika masomo ili kuepuka matokeo mabaya katika mtihani
wa mwisho.
Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) juzi lilitangaza matokeo ya mtihani
wa kidato cha nne kwa mwaka 2016 na kubainisha ufaulu wa jumla kwa
watahiniwa wa shule kuongezeka kwa asilimia 2.44, idadi ya watahiniwa
waliopata alama za kuwawezesha kuendelea kidato cha tano kuwa chini kwa
miaka mitatu mfululizo.
Hata hivyo, katika matokeo hayo, shule sita za mkoa wa Dar es Salaam
zimekuwa miongoni mwa shule 10 za mwisho kitaifa. Shule hizo ni Kitonga,
Nyeburu, Kidete, Mbopo, Mbondole na Somangila Day, ambazo katika kundi
hilo zimo pamoja na Masaki (Pwani), Dahani (Kilimanjaro), Ruponda
(Lindi) na Makiba (Arusha).
Wanafunzi wasio na uwezo
Gazeti hili jana na juzi lilitembelea baadhi ya shule hizo na kuzungumza
na walimu, watendaji wa elimu na watendaji wa serikali wa kata pamoja
na wanafunzi, na katika mazungumzo hayo, zimetajwa sababu mbalimbali
zikiwamo za kuchukuliwa kwa wanafunzi wanaopata alama za chini darasa la
saba, na suala la umbali kwa wanafunzi kutoka wanakoishi hadi shule
walizopangiwa kusoma.
Shule zilizotembelewa ni Kitonga, Mbondole zilizopo katika Kata ya
Msongola na Sekondari ya Nyeburu iliyopo katika Kata ya Chanika, zote
katika Manispaa ya Ilala.
Mmoja wa walimu katika shule hizo, alisema kumekuwa na tabia ya kupeleka
wanafunzi wenye ufaulu wa chini ya alama zinazotakiwa za ufaulu wa
darasa la saba ambazo ni 250, hivyo kusababisha kuchukua wanafunzi wasio
na uwezo darasani.
“Sababu zinaweza kuwa nyingi, lakini hili la kuchukua wanafunzi ambao
walifeli darasa la saba kiasi cha kushindwa kumudu masomo ya sekondari
lipo. Mwanafunzi anatakiwa kupata alama 250, lakini wapo wanafunzi ambao
wamepata hata alama sabini wamechukuliwa,” alisema mmoja wa mkuu wa
shule msaidizi wa shule mojawapo ambaye alikataa kutaja jina lake.
Kama ilivyokuwa kwa mwalimu huyo, mmoja wa wenyeviti wa kata hizo naye
alikataa kutaja jina, lakini alieleza kuwa kumekuwapo na wanafunzi
wanaopelekwa katika shule hizo wakiwa wamepata alama za chini sana
katika mitihani ya kumaliza darasa la sababu.
Umbali watajwa
Suala la umbali pia lilitajwa kama sehemu ya changamoto zilizosababisha
matokeo hayo mabaya kwa wanafunzi wa shule hizo za Dar es Salaam. Katika
Sekondari ya Kitonga, walimu walikutwa wakiwa kwenye kikao na viongozi
wa kata kujadili changamoto zilizofanya shule hiyo kushika nafasi ya
mwisho.
Akizungumza baada ya kumaliza kikao, Mratibu wa Elimu katika Kata ya
Msongola, Venance Mwakilembe alisema bado anafanya utafiti katika shule
za kata hiyo zilizofanya vibaya kufahamu sababu ya kwa nini wamepata
alama hizo na akipata majibu atapeleka sehemu husika.
Lakini alidai kwa ujumla changamoto kubwa ni watoto kukaa mbali na shule
na hakuna mabweni hivyo kutumia muda mrefu kufika shule na kurudi
nyumbani.
“Kutokana na usimamizi mbovu wa wazazi ambao wamekuwa wagumu
kushirikiana na walimu haijulikani watoto wanafanya nini njiani, lakini
wamekuwa watoro na kuibuka kujisajili kufanya mtihani wa mwisho wa
kidato cha nne,” alisema Mwakilembe.
Aliweka wazi kuwa katika kikao cha wazazi cha mwisho kwa watoto 200
waliopo shuleni, walifika wazazi 20 pekee huku kuna wakati wazazi
waliwapangia wanafunzi vyumba bila kuwa na uangalizi kwa sababu ya umri
wao waliishia katika matendo machafu, jambo ambalo shule ililazimika
kupiga marufuku.
Katika shule hiyo yenye ikama nzuri ya walimu 26, wana maabara na
masuala mengine ya kitaaluma yakiwa vizuri, lakini changamoto ni ya
umbali wanaosafiri watoto. Jirani wa shule hiyo, Hassan Waziri anasema
serikali inatakiwa kuhakikisha wanafunzi wanaosoma hapo wawe wanakaa
karibu au vinginevyo wajenge mabweni.
Wanafunzi waishia njiani
Katika Shule ya Sekondari ya Ndombole, mmoja wa walimu aliyekataa kutaja
jina alisema wanafunzi hadi kufika maeneo hayo ambayo yako karibu na
shule ya Kitonga, wanatoka maeneo mbalimbali ya jiji, lakini anaeleza
kuwa kuanzia watakaomaliza kidato cha nne mwaka huu walianza kupangiwa
wanaoishi karibu na shule.
Inaweka bayana kuwa mwanafunzi hadi kufika shuleni anapanda daladala nne
kwa anayetokea Buguruni mpaka Gongo la Mboto, Chanika, Mvuti na mwisho
anapanda yanayoenda Mbagala na kushuka shuleni anapolazimika kutembea
kilometa tatu au kuchukua bodaboda kwa Sh 1,000.
Anaeleza kuwa umbali huo wa shule umesababisha wanafunzi wengi kuwa
watoro na kuishia vichakani huku wengine wa kike wakidanganywa na
waendesha bodaboda.
Alisema kutokana na changamoto hiyo, walilazimika kutafuta basi la shule
lililokuwa likibeba wanafunzi kutoka Buguruni mpaka shuleni na kulipa
Sh 2,000 kwa siku, lakini baadhi ya wazazi walikuwa wagumu kulipa kwa
kusema ni nyingi hivyo kuacha huduma hiyo.
Alieleza kuwa wanafunzi waliofaulu kwa alama 240 hadi 245 darasa la saba
ndiyo wamepata daraja la tatu huku wengine wakifeli kutokana na kuvutwa
na waliofeli ambao ni wengi; kama ilivyokuwa kwa shule nyingine
zilizovurunda kwa kuchukua wenye alama za chini sana.
Mmoja wa watendaji wa kata hiyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa kwa
madai ya kuwa siyo msemaji wa shule hizo, aliweka bayana kuwa
alitembelea moja ya shule na kubaini kuwepo mwanafunzi wa kidato cha
tatu asiyeweza kuandika kwa ufasaha sentensi ya Kiswahili.
Alisema changamoto ya umbali na kupelekewa wanafunzi waliofanya vibaya
mtihani wa darasa la saba nayo ni changamoto kwani wapo waliofaulu
mtihani huo kwa wastani mzuri wamepata daraja la tatu.
Katika Sekondari ya Kidete iliyopo kilometa 10 kutoka daraja la Mwalimu
Julius Nyerere katika Wilaya ya Kigamboni, inaeleza kuwa ufaulu mdogo wa
wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza shuleni hapo na umbali wa shule
kwa wanafunzi ni changamoto shuleni hapo.
Mwalimu wa shule hiyo aliyekataa kutaja jina, alisema kutokana na umbali
wanafunzi wengi hufika kwa kuchelewa muda wa masomo kwani wengi
wanatokea Yombo Buza na maeneo mengine ya wilaya ya Temeke kwani
wanatoka nyumbani saa 10 au 11 alfajiri na kuondoka shuleni saa 8:30
mchana.
Mzazi, mwanafunzi wasifu walimu Katika Sekondari ya Nyeburu, mwanafunzi
wa kidato cha pili, Roneco Nziku alisema walimu wanao na wamekuwa
wakifundisha vizuri isipokuwa tatizo lipo kwa wanafunzi.
Alisema licha ya kuwa matokeo hayo yanakatisha tamaa, lakini anaamini
akijitahidi kusoma kwa bidii hasa masomo ya sayansi anayoyapenda
atafanya vizuri kwani shule hiyo ina maabara tatu za masomo ya Kemia,
Baolojia na Fizikia isipokuwa tatizo lipo kwa wanafunzi kutozingatia
kile wanachofundishwa.
Nziku alisema umbali wa shule kwa wanafunzi ni changamoto kwani wanafunzi wengi hutoka Buguruni na maeneo mengine ya mbali.
Mwananchi anayeishi jirani na shule hiyo, Severino Wami alisema
wanafunzi wenyewe wanaonekana hawana nidhamu, lakini pia hawaonekani
kama ni watu wanaopenda kusoma kwani huwa hawafiki shule wanakwenda
kukaa kwenye mabanda ya mtaani.
“Tunasikia kuna banda moja lipo mtaani ambapo wanafunzi baadhi huishia
huko, kitu kingine tunasikia wengi wanatoka maeneo ya mbali kama
Buguruni, atatoka saa ngapi arudi ajisomee na kesho awahi, mazingira
magumu,” alisema Wami.
Pia alisema hata wazazi wanaweza wakawa ni sababu ya wanafunzi kufeli
kwa sababu hawana muda wa kufuatilia viwango au maendeleo ya watoto wao
darasani au kama anasoma anaporudi nyumbani.
Naye mzazi wa mtoto Michael Kitumbo anayesoma kidato cha tatu kwenye
shule hiyo, Subira Kitumbo, alisema haoni kama walimu wana matatizo
kwenye shule hiyo kwani siku zote wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa
wazazi kushirikiana nao katika kuhakikisha mtoto anafanya vizuri.
Viashiria vilionekana mapema Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Kaimu Ofisa Elimu wa Mkoa, Janeth Nsunza alisema wakuu wa shule hizo
zilizofanya vibaya wametakiwa kujieleza na walianza kutoa maelezo, ikiwa
ni sehemu ya hatua walizoanza kuzichukua.
“Mkoa umepokea matokeo hayo kwa masikitiko kwani umekuwa ni kinyume cha
matarajio yetu na serikali kwa ujumla kwa kuwa serikali imekuwa
ikisisitiza utoaji wa elimu msingi bora kwa wote,” alisema Nsunza.
Alisema viashiria vya matokeo mabaya kwa shule hizo yalianza kuonekana
katika matokeo ya mtihani wa majaribio (Mock), jambo ambalo liliwafanya
wakurugenzi kuwaandikia barua wakuu wa shule hizo kuongeza juhudi katika
masomo ili kuepuka matokeo mabaya katika mtihani wa mwisho.
“Wakati wa mtihani wa Mock, shule hizi zilionesha viashiria vya matokeo
mabaya na wakurugenzi waliwaandikia barua wakuu wa shule na kuwataka
kuhakikisha wanafanya jitihada ili kuhakikisha shule zao zinakuwa na
matokeo mazuri. Lakini tumeona bado hali imekuwa tofauti hawa wanatoa
maelezo na mkoa utatangaza hatua za kuchukua baada ya kukamilisha,”
aliongeza ofisa huyo.
Nsunza alisema wanafunzi waliofeli ni 619 ambao ni sawa na asilimia 1.1
kati ya wananfunzi 55,980 waliosajiliwa kufanya mtihani mwaka 2016.
Aliongeza kuwa shule hizo sita zilizoshika nafasi ya mwisho ni miongoni
mwa shule 128 zilizojengwa kwa nguvu za wananchi katika manispaa za jiji
hilo.
Wizara yatoa neno
Akizungumzia kufanya vibaya kwa shule hizo, Kaimu Kamishna wa Elimu
kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi,
Nicolas Buretta alisema ipo haja ya kukaa pamoja na mamlaka za Mkoa wa
Dar es Salaam ili kufanya uchambuzi wenye kutafuta sababu.
Buretta alisema suala hilo linahitaji utulivu, sio la kuzipata sababu za
kufeli kwa shule hizo kwa haraka, bali inahitajika kuwatafuta wadau
mbalimbali wa elimu ili kuchambua na kupata kiini cha suala hilo.
“Suala la kuanguka kwa shule hizo sio la kulipatia jibu kwa haraka, ni
jambo linalotaka utulivu ili kuweza kuwashirikisha wadau wote na
kutafuta sababu za kufeli kwa shule hizo,” alifafanua Kaimu Kamishna wa
Elimu.
Kibaha yaibeba serikali Kwa upande mwingine, shule kongwe ya Kibaha
mkoani Pwani ni miongoni mwa shule 20 bora, ambayo imeshika nafasi ya 16
kati ya shule 3,280 za sekondari nchini.
Kwa mujibu wa takwimu za viwango vya ufaulu zilizowekwa kwenye tovuti ya
Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Kibaha iliyoko Mkoa wa Pwani
wanafunzi wamepata daraja la kwanza hadi la nne, na hakuna mwanafunzi
aliyefeli.
Kibaha imepanda kwani mwaka 2015 ilishika nafasi ya 69 na mwaka 2014
ilikuwa ya 87. Wakati Kibaha ikiwa ya kwanza kwa ufaulu bora kwa shule
za serikali, imefuatiwa na shule ya wanafunzi wenye vipaji ya Mzumbe ya
Morogoro iliyoshika nafasi ya 27, na haina mwanafunzi aliyefeli.
Mwaka 2015, Mzumbe ilikuwa nafasi ya 71 na mwaka 2014 ilikuwa ya 56.
Shule ya wasichana ya Kilakala imeshika nafasi ya 28 na hakuna
mwanafunzi aliyefeli. Mwaka 2015 ilishika nafasi ya 94 na mwaka 2014
ilikuwa ya 96.
Tabora Boys ikishika nafasi ya 41 na kufuatiwa na Ilboru ya Arusha iliyo
nafasi ya 42. Shule zingine na nafasi zao kwenye mabano ni shule ya
wasichana Tabora (114), Msalato (129), Songea Boys (201), Bwiru (214) na
Moshi Sekondari (226).
Kwa upande ya 20 za mwisho, bado inaonekana shule za serikali ndizo
zilizoko kwenye eneo hilo kwa kuwa na wastani hafifu. Shule zingine 10
zinazofuatiwa zile zilizotangazwa na Necta ni Mtombozi (Morogoro),
Mkikira (Mara), Ndangalimbo na Mnero (Lindi), Ngiresi (Arusha), Piki
(Kaskazini Pemba), Kazamoyo (Pwani), Zingiziwa na Sangara (Dar es
Salaam), Mugango (Mara) na Mkera (Dar es Salaam).
0 comments:
Post a Comment