Siku mbili baada ya kuwa madarakani, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga amesema hakuna mtu
atakayepona baada ya kubainika akitakatisha fedha zilizopatikana kwa
njia ya dawa za kulevya.
Sianga amesema hayo katika mkutano ulioitishwa na Mkuu wa mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda ambapo pia alikabidhiwa na Makonda majina 97 ya
watu wanaojihusisha na dawa hizo.
Kamishna huyo amesema atakayefanya biashara ya dawa za kulevya au
utakatishaji wa fedha atachukuliwa hatua kwa sababu sheria mpya ya
udhibiti inawapa uwezo wa kukamata hadi mali ambazo atakayepatikana na
hatia amezichuma.
Kamishna wa Intelijensia wa mamlaka hiyo, Frederick Kibuta amesema
katika kutekeleza majukumu ya taasisi hiyo, watazingatia sheria katika
kila hatua.
Amewataka wananchi kufahamu sheria kwa sababu kutokujua hakutoi nafasi ya kuzivunja.
“Popote walipo tutawafikia na tutawachukulia hatua, hakuna atakayebaki salama katika hili,” amesema Kibuta.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Makonda amemuomba Spika wa Bunge,
Job Ndugai aweke kipimo maalumu kitakachokuwa kinawapima wabunge kabla
hawajaingia bungeni ili wabainike kama wanatumia dawa za kulevya au la.
“Kaka yangu Ndugai alisema ana nia ya kuweka kifaa maalumu kuwapima
wabunge kama wanatumia dawa za kulevya au la, hivyo atimize nia yake
hiyo ili kama na huko wapo tuwanyofoe,” amesisitiza Makonda.
0 comments:
Post a Comment